Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- katika kikao hicho, mbali na kujadili hali ya sasa ya eneo na uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa haya mawili ya Kiislamu na ndugu, pia walizungumzia masuala yanayohusu wahajiri, wanafunzi wa Afghanistan wanaosoma Iraq na suala la viza baada ya Arubaini.
Taarifa zinaeleza kuwa mkutano huu umefanyika wakati ambapo Haji Muhaqiq alikuwa amezuru Karbala Tukufu kwa ajili ya kushiriki ziara ya Arubaini na sambamba na ibada hiyo, amefanya pia mikutano na baadhi ya viongozi wa Iraq.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili ziliangazia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kidini, kiutamaduni na kisiasa baina ya nchi hizi mbili, pamoja na kushughulikia changamoto zinazowakabili wahajiri na wanafunzi wa Afghanistan nchini Iraq.
Hata hivyo, sambamba na mikutano hiyo, kumekuwepo na malalamiko makubwa miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Afghanistan kuhusu ukosefu wa mipangilio na uratibu mzuri. Changamoto hizo zilisababisha maelfu ya wapenzi wa Imam Hussein (a.s) kutoka Afghanistan kushindwa kushiriki katika maadhimisho makubwa ya Arubaini huko Karbala mwaka huu.
Wengi wanaamini kuwa ucheleweshaji katika mchakato wa utoaji viza, usimamizi hafifu na masharti magumu yasiyo ya lazima yamewakatisha tamaa na kuumiza nyoyo za wapenda Ahlul-Bayt (a.s), na hatimaye kuwanyima Wafghan fursa ya kushiriki katika mkusanyiko mkubwa zaidi wa kidini duniani.
Your Comment